loader

Namna ya Kutumia Twenzao

Fig. 1.7: Wasafiri wanne wenye furaha wakichati kwenye safari ya Twenzao

Twenzao ni app inayomuunganisha mwenye gari binafsi na abiria wanaoenda muelekeo wake. App inapatikana Play Store na App Store, njia rahisi zaidi kuipata ni kwa kubonyeza link za app zilizoko kwenye homepage ya tovuti yetu hii, link zitakupeleka moja kwa moja kwenye app katika store husika.

Watumiaji wa pande zote mbili (dereva na abiria) wanahitaji kufungua akaunti kwenye aplikesheni ya Twenzao kwa madhumuni ya kuwatambua na pia kuwezesha mawasiliano kati yao. Mara tu akaunti itapofunguliwa, madereva wanaweza kuchapisha safari zao ambazo zitaonekana kwa yeyote anayetafuta safari kwenye Twenzao. Abiria anachotakiwa kufanya ni kuonyesha anapotoka, anapoenda na tarehe ya safari, hapo anaweza kuona safari zinazoendana na kile alichokitafuta.

Ni juu ya wasafiri (abiria na dereva) kukubaliana kuhusu pa kukutania, endapo watahitaji kukutana eneo tofauti na lile ambalo dereva alionyesha wakati wa kuchapisha safari yake. Maeneo ya kukutana yanatakiwa kuwa salama na rahisi kufikiwa na wote. Hizi ni sehemu kama makanisa, vituo vya mafuta, vituo vya mabasi, maduka maarufu, misikiti, n.k.

Mawasiliano kati ya dereva na abiria wake yanawezekana kupitia njia mbili, kuchati kupitia Twenzao, au kupitia nambari ya simu - nambari za simu za dereva na abiria zinaonekana kwa kila mmoja mara tu booking ya safari baina yao inapokuwa imethibitishwa.

Ukiwa abiria, ni kawaida kuwa kwenye safari yako ya Twenzao kutakuwa na abiria wengine waliobuku safari hiyo hiyo kupitia Twenzao kama wewe. Vile vile, mtu mmoja anaweza kubuku zaidi ya siti moja kulingana na upatikanaji wa siti kwenye gari husika. Sio kwa sababu tu najaribu kukushawishi utumie Twenzao, ila ni kweli, Twenzao imetengenezwa kwa namna ambayo inajieleza yenyewe, na utaelewa haraka na kwa urahisi zaidi endapo ukianza moja kwa moja kuitumia badala ya kujichosha na maelezo haya marefu. Lakini ukiamua kuendelea kusoma, sawa acha tuendelee, napenda sana kuandika ...

Baada ya safari, pande zote mbili zinapata nafasi ya kutoleana maoni ("reviews"), na maoni haya yataonekana wazi kwa watumiaji wengine wa Twenzao. Huna haja ya kuwa na wasiwasi kuwa mtu atakutolea maoni kuendana na vile ulivyomuelezea yeye, kwa sababu maoni yako hayataonekana mpaka pale ambapo yeye pia atakuwa ameshatoa maoni yake juu yako, au baada ya kumalizika kwa kipindi cha wiki mbili. Mfumo wa maoni unatusaidia kuboresha huduma zetu na kuhakikisha usalama wa wateja wetu, na pia husaidia wengine kufanya maamuzi sahihi endapo wanataka kusafiri na mtu fulani.

Kumbuka kutafuna vipochopocho vyote utakavyovikuta kwenye gari (Natania tu, lakini kweli, kushea kunaweza kumshawishi mtu kukupa maoni mazuri zaidi :P)!!