loader

Pata Kutujua

Naapa utapendezwa na haiba yetu wana Twenzao. Sisi ni watu wa kawaida sana, hatuna makuu, kwanza ni vichekesho tu sisi. Yaani angalia hata rangi zetu, sisi ni wa zambarau lol! Kwa juu juu, sisi sio watu siriasi, njoo uchill nasi, ila kikazi, labda sisi ndio watu siriasi zaidi kwenye sayari hii, huduma yetu ya Twenzao iko kwenye ligi ya application za viwango vya hali ya juu zaidi kwenye gemu hili.

Amo, mwanzilishi wetu, ni mtu simpo tena mwenye nishai ambaye hana kitu kingine akilini mwake zaidi ya magari, barabara na programming. Anaweza kukutajia miji na vijiji vyote hata vile vidogo kabisa vilivyo kando ya barabara kuu ya Mwanza-Dar, njia ambayo ndiyo ruti yake kipenzi zaidi.

Halafu kuna Bube. Ningeweza kukuambia mengi kuhusu Bube, lakini nahisi yote ambayo ningekwambia juu yake yanaweza kunigharimu ajira yangu hapa Twenzao. Unachopaswa kujua ni kwamba Bube ndiye anayesimamia masuala ya kisheria ya kampuni, na kama wakili mashuhuri, ana rekodi ya kushinda kesi ambazo wengi katika uwanja wa sheria walikuwa wamezipotezea matumaini.

Unapozungumzia Twenzao, huwezi kukosa kumtaja Khadi. Amekuwepo tangu mwanzo wakati bado Twenzao ilikuwa mzaha tu uliozungumziwa kwenye meza ya chakula mpaka ilipofikia leo kuwa platform ya kwanza na ya pekee Tanzania inayowezesha watu kuchangia usafiri wa magari binafsi! Khadi anahusika sana na uhakiki wa software, yaani "software testing" na pia anasimamia mahusiano ya kampuni na wateja.

Mandela ana jukumu la kipekee sana Twenzao. Ni rahisi kupuuza jukumu lake, lakini naweza kukuambia bila mchango wake Twenzao isingesimama leo. Ili kutoa sifa pale inapostahili, Mandela ndiye aliyebuni jina letu la "Twenzao". Kwa sasa naomba kuficha jukumu lake haswa, lakini waweza kumwita "Mwanaharakati".

Apro ndiye kiongozi wa kiroho wa Twenzao, na amehakikisha kuwa pepo wabaya hadi sasa wamekaa pembeni. Hebu wewe fikiria kiongozi wa kiroho anayeweza kutest software kitaalamu, na unachopata ni nguvu ya ajabu ambayo mchango wake utaandikwa kwenye vitabu vya Historia vya vitukuu zetu.

Adi ni msumbufu wa kifikra, na amini nakwambia unahitaji wasumbufu hawa katika maisha yako. Unajua wakati ule ambapo kila mtu miongoni mwa rafiki zako ameridhia kula KFC halafu akajitokeza mmoja anayesisitiza kutafuta shamba la kuku lililo karibu zaidi ili kufaidi moja kwa moja kutoka kwa mkulima? Huyo atakuwa Adi, msumbufu wa kifikra. Ulimwengu hubadilishwa na wasumbufu kama hawa.

Hawa ndio watu wanaotengeneza kiini cha familia ya Twenzao. Pindi majukumu yetu yatakapokuwa yamepungua, tutatenga wakati maalum kupiga picha za wanandugu hawa wa Twenzao. Tafadhali ambatana nasi katika safari hii, nakuhakikishia kuwa utaipenda!

NB: Pengine unajiuliza ni nani huyu aliye mwandishi wa habari hii!? Kwa sasa nakuachia chemsha bongo hiyo.